Meneja akamatwa kwa kuharibu gari la mwanamuziki Uganda

Inaripotiwa kwamba Januari 3, 2025, Awio na walinzi 6 aliokuwa amekodisha walivamia mwanamuziki Ogwang Walter maarufu kama Lil Square, na kuharibu gari lake aina ya Toyota Max 2 Grand la rangi nyeupe.

Marion Bosire
2 Min Read
Lil Square na Awio Scrap Dealer

Isaac Awio, maarufu kama Awio Scrap Dealer ambaye hujihusisha na kazi za kusimamia wanamuziki nchini Uganda alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kushambulia mwanamuziki na kuharibu gari lake.

Maafisa wa kituo cha polisi cha Lira walimkamata Awio wa umri wa miaka 28, pamoja na mlinzi wake Erick Odyeny wa miaka 28.

Inaripotiwa kwamba Januari 3, 2025, Awio na walinzi 6 aliokuwa amekodisha walivamia mwanamuziki Ogwang Walter maarufu kama Lil Square, na kuharibu gari lake aina ya Toyota Max 2 Grand la rangi nyeupe.

Msemaji wa polisi katika eneo la Kyoga Kaskazini Jimmy Patrick Okema alisema kwamba video iliyosambazwa mitandaoniilimwonyesha Awio akiegesha gari lake mbele ya gari la Lil Square.

Anaonekana akianzisha mashambulizi hayo yaliyojumuisha kuharibu kioo cha mbele.

Polisi walichunguza kisa hicho na walipojaribu kukamata mshukiwa akajaribu kuruka ukuta wa eneo la burudani la Glass Lounge.

Hatimaye walifanikiwa kukamata wawili hao na washukiwa wengine bado wanasakwa. Awio alikuwa meneja wa Lil Square, lakini haijulikani walikuwa wanazozania nini.

Mwezi Machi mwaka jana, Lil Square kupitia Facebook alitangaza kukatika kwa mkataba kati yake na Awio huku akimshukuru kwa ufanisi aliomsaidia kuafikia katika muda mfupi.

Alitaja sababu za kibinafsi katika kuafikia uamuzi huo na kutoa nambari yake ya simu ili wale ambao wangetaka kufanya kazi naye wawasiliane naye moja kwa moja.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *