Meli za kivita za Marekani zilishambuliwa kwa makombora na droni, mashambulizi yaliyotekelezwa na wapiganaji wa Houthi zilipokuwa zikiondoka pwani ya Yemen.
Pentagon imethibitisha suala hilo huku kundi la Houthi likisema kwamba lilishambulia meli ya kubeba ndege ya Abraham Lincoln na nyingine mbili za kuharibu makombora.
Msemaji wa Pentagon Patrick Ryder alisema Jumanne kwamba majeshi ya Marekani kutoka kikosi kikuu yalifanikiwa kukabili mashambulizi ya Houthi yanayoungwa mkono na Iran katika mapito ya Bab al-Mandeb yanayounganisha bahari ya shamu na ghuba ya uajemi.
Ryder aliambia wanahabari kwamba meli mbili za kuharibu makombora zilishambuliwa na droni nane, makombora matano ya kuharibu meli na mengine matatu ya kuharibu meli zinazoendelea kusonga.
Kulingana naye, droni hizo pamoja na makombora ya Houthi vilikabiliwa na kushindwa na hakuna meli iliyoharibiwa wala mhudumu kuumizwa.
Ryder alifafanua kwamba hafahamu kuhusu kushambuliwa kwa meli ya kubeba ndege ya Marekani ya Abraham Lincoln.
Wapiganaji wa Houthi walitangaza mapema Jumanne kwamba walikuwa wametekeleza oparesheni mbili dhidi ya wanamaji wa Marekani iliyodumu saa nane.