MCSK yamtaka MC Jessy alipie leseni ya onyesho lake

MC Jessy haelewi ni kwa nini anatakiwa kulipa mashirika ya muziki ilhali onyesho lake ni la vichekesho.

Marion Bosire
1 Min Read

Shirika la hakimiliki za muziki nchini MCSK limemtaka mchekeshaji MC Jessy alipe shilingi laki mbili ili apatiwe leseni ya kuendesha onyesho lake.

Jessy alichapisha nakala ya ankara aliyotumiwa na MCSK jana Disemba 9, 2024 kabla ya kuandaa onyesho hilo ambalo amelipa jina la “+ or—40”.

Kando na MCSK, Muungano wa waandaaji muziki KAMP) na ule wa haki za watumbuizaji PRISK ni wahusika katika kudai malipo hayo.

Mchekeshaji huyo anasema onyesho lake ni la vichekesho na haelewi ni kwa nini anadaiwa na mashirika yanayohusika na muziki.

Anasimulia jinsi ametia bidii katika kutangaza onyesho hilo ambalo limepangiwa kuandaliwa kesho Jumatano Disemba 11, 2024 jioni katika ukumbi wa Skate City jijini Nairobi, kisha anakumbana na matatizo kama haya.

Msanii huyo alifichua kwamba ametishiwa kukamatwa iwapo hatalipa pesa hizo.

Alisema pia kwamba hatalipa pesa hizo huku akiwataka wawasilishaji wa ankara hiyo watekeleze vitisho vyao, akishangaa ni kwa nini mashirika kama hayo hayawaungi mkono badala ya kuwadhalilisha.

Kulingana na bango la kutangaza onyesho hilo, MC Jessy atakuwa mchekeshaji pekee atakayetumbuiza katika kile anachorejelea kama “One Man, One Night, One Mic”.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *