Raphael Dwamena mchezaji soka mzaliwa wa Ghana ambaye aliwahi kuichezea timu ya taifa hilo amefariki akiwa na umri wa miaka 28.
Dwamena alikata roho jana uwanjani akiwa anachezea timu ya KF Egnatia ya Albania, timu aliyojiunga nayo Disemba 2022.
Mchezaji huyo alianguka dakika ya 24 ya mechi ya ligi kuu ya Albania kati ya KF Egnatia na Partizani na kwa wakati huo timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Shirikisho la soka nchini Ghana lilitangaza taarifa hiyo ya tanzia likiahidi kusimama na familia ya mwendazake wakati huu wa majonzi.
Video iliyosambazwa mitandaoni inamwonyesha Dwamena akianguka huku wachezaji wa timu zote mbili wakikimbilia alikokuwa.
Alihudumiwa na wahudumu wa kiafya kabla ya kubebwa na ambulensi iliyokuwa imeletwa uwanjani.
Dwamena aliwahi kuanguka tena uwanjani Oktoba 2021 kwenye mechi kati ya timu yake ya wakati huo Blau-Weiß Linz na Hartberg kwenye ligi ya Austria lakini akahudumiwa akawa sawa na kurejelea mchezo.
amechezea vilambu mbali mbali vya soka nchini Uhispania, Uswizi, Austria na Denmark.