Mchekeshaji na mwigizaji wa Nigeria AY ametumia akaunti yake ya Instagram kusherehekea maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya binti yake, anapotimiza umri wa miaka mitatu.
Alitumia maneno ya upendo, imani na ya kifamilia kumsherehekea msichana huyo kwa jina Adele Ayomide Makun.
AY alimtaja binti yake kuwa ‘mwanga unaong’aa’ katika maisha yake na ‘zawadi ya thamani’ anayosema ilimjia baada ya subira ya miaka 13.
Baba huyo alikuwa mwenye shykrani kwa muda aliopata wa kuwa na bintiye huku akilalamika kwamba siku hizi huwa hamwoni mara kwa mara kama awali.
“Hata ingawa matukio kadhaa yasiyoweza kurekebika yameghubika kile ambacho awali kiliitwa familia, jua kwamba unapendwa na mamako na mimi.” aliandika AY akirejelea tukio la kutengana na mke wake Mabel.
Baba huyo wa watoto wawili aliendelea kusifia hulka za mwanawe kama kicheko kizuri ambacho humfurahisha kila mmoja anayehusiana naye.
Aliangazia pia jinsi ujio wa bintiye ulimwenguni ulijaza moyo wake na furaha na kurejesha imani yake katika uwezo mkubwa wa upendo na amani.
AY alidhihirisha furaha kuhusu mustakabali wa binti yake akisema anasubiri kuona mengi makuu atakayoafikia maishani.
Wafuasi wake nao walimtakia msichana huyo mema anapotimiza umri mpya.
Mama ya mtoto huyo Mabel Makun naye alichapisha picha zake na kumwandikia, “Siku njema ya kuzaliwa unayependwa zaidi na Mungu, Nyota ya mbinguni inayong’aa Ayomide MAKUN. Tunashukuru Mungu kwa kutuheshimisha na uwepo wako kwenye maisha yetu.”