Mbunge wa zamani wa Tanzania Selemani Saidi Ally Bungara afariki

Bungara ambaye wengi walimfahamu kwa jina la utani "Bwege", alipelekwa hospitalini kwa matibabu ya kawaida jana lakini akazidiwa na kufariki.

Marion Bosire
1 Min Read

Selemani Saidi Ally Bungara ambaye alihudumu kama mbunge wa eneo la Kilwa Kusini nchini Tanzania mwaka 2005 hadi 2020 amefariki.

Bungara ambaye wengi walimfahamu kwa jina la utani “Bwege”, alipata kufahamika nje ya Tanzania kutokana na usemi wake maarufu wa “Olisikia wapi?”.

Alitamka maneno hayo katika mahojiano na wanahabari wakati siasa zilikuwa zimepamba moto nchini Tanzania mwaka 2020.

Mbunge huyo wa zamani anaripotiwa kufariki jana Machi 30, 2026 mchana katika hospitali moja ya kibinafsi huko Kigamboni, Dar es Salaam.

Kakake aitwaye Abbas S.A. Bungara aliambia wanahabari kwamba marehemu alifikishwa hospitalini kwa matibabu ya figo almaarufu Dialysis kama kawaida lakini akakumbana na mauti.

Abbas alisema hiyo jana kwamba familia ilikuwa ikiangazia mipango ya mazishi na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baadaye. Alifahamisha umma pia kwamba msiba ni nyumbani kwake huko Temeke.

Awali, marehemu Bwege alikuwa mwanachama wa chama cha CUF kabla ya kujiunga na chama cha ACT Wazalendo.

Hivi karibuni alitangaza kwamba amejiunga na CHADEMA ingawa mchakato rasmi wa kukabidhiwa kadi ya chama hicho ulikuwa haujakamilika.

Bungara, aliyekuwa na umri wa miaka 64, amekuwa akiugua kwa muda ambapo maradhi yalisababisha mguu wake kupooza kiasi cha kumsababisha atumie kiti cha magurudumu.

Share This Article