Mbunge wa zamani Lawrence Sifuna ameaga dunia

Marion Bosire
1 Min Read

Lawrence Sifuna ambaye aliwahi kuhudumu kama mbunge wa maeneo ya Kanduyi na Bumula ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 78. Hayo ni kwa mujibu wa mpwa wake ambaye ni Seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna.

Seneta Sifuna alitangaza hayo kupitia mitandao ya kijamii akielezea kwamba Lawrence alikata roho usiku wa kuamkia leo akiendelea kupokea matibabu katika hospitali moja mjini Eldoret.

Mzee huyo aliugua kiharusi hivi maajuzi.

Seneta Sifuna anasema kama familia, wanashukuru kwa jumbe za kuwafariji ambazo wanaendelea kupokea.

Marehemu Sifuna ndiye alikuwa mbunge wa kwanza wa eneo bunge la Bumula.

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza Novemba 8, 1979 na akachaguliwa tena mwaka 1983.

Alishindwa na Maurice Makhanu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1988 wakati jina la eneo bunge la Bungoma Kusini lilibadilishwa na kuwa Kanduyi.

Kitaaluma, alikuwa mhasibu.

Share This Article