Mbunge wa Mukurweini John Kaguchia leo Jumatano alifikishwa katika Mahakama Kuu akikabiliwa na mashtaka ya kutoa semi za chuki.
Kaguchia alikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) jana Jumapili kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa kisiasa eneo la Kieni, kaunti ya Nyeri.
Mbunge huyo alikamatwa baada ya kukesha usiku kucha katika afisi za chumba kimoja cha habari, alikoshiriki mahojiano.
Kaguchia, ambaye ni mwandani wa kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua, amekuwa akimulikwa na vyombo vya usalama baada ya kudaiwa kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa kisiasa Jumamosi iliyopita.
Ni matamshi yanayodaiwa kuwaonya wakazi wa Mlima Kenya dhidi ya kumpigia kura Rais William Ruto wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, Kaguchia amekanusha madai hayo akisema alinukuliwa vibaya.
Mbunge huyo alikamatwa wakati ambapo Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano inawachunguza baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa madai ya kutoa matamshi ya chuki.
Wanaochunguzwa ni pamoja na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua na Mawaziri Aden Duale wa Afya na Geoffrey Ruku wa Utumishi wa Umma.