Mbunge wa Lurambi, Titus Khamala, ameweka wazi kwamba eneo la Magharibi halitakubali nafasi yoyote chini ya ile ya Naibu Rais katika serikali ijayo ya mwaka 2027.
Akihutubu katika Shule ya Upili ya Shieywe wakati wa utoaji wa hundi za basari zenye thamani ya shilingi milioni 55, Khamala alisisitiza kuwa wakaazi wa Magharibi wamechoshwa na hali ya kuwaunga mkono viongozi wa jamii nyingine, lakini mwishowe wakijipata upande wa upinzani.
Licha ya viongozi wa Magharibi kuamua kwa kauli moja kumuunga mkono Rais William Ruto katika azma yake ya kuwania muhula wa pili, Khamala alisisitiza kuwa ni lazima Ruto amteue mmoja wao kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa 2027.
Mbunge huyo pia alitoa wito kwa mchakato wa uteuzi wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwa wa wazi na wa haki ili kuhakikisha uchaguzi unaoaminika mwaka 2027.
Kauli ya Khamala iliungwa mkono na Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, ambaye alizungumza katika hafla tofauti katika eneo bunge lake.