Mbunge Peter Salasya kufikishwa mahakamani Jumanne

Tom Mathinji
1 Min Read

Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne ijayo kufuatia madai ya mashambulizi wakati wa mazishi kwenye Kaunti ya Kakamega siku ya Ijumaa.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi, mbunge huyo alikamatwa kuhusiana na tukio hilo, ambapo walinzi wake wawili wanadaiwa kufyatua risasi hewani.

Baadaye aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 50,000.

Kanda ya video iliyonakili tukio hilo, ilimnasa Salasya akiwahutubia waombolezaji waliokusanyika wakati wa hafla hiyo.

Dakika chache baada ya hotuba yake, umakini wa Salsaya ulikuwa kwa mtu mmoja ambaye hakunaswa na kamera ambaye mbunge huyo alimsihi mara kwa mara aketi ili aendelee na hotuba yake.

Licha ya maagizo yake, mwanamume huyo, anayesemekana kuwa ni mwakilishi Wadi katika eneo hilo, aliyenuia kuhutubu katika hafla hiyo aligoma kutii agizo la Mbunge huyo, na kumfanya mbunge huyo kumzaba kofi.

Aidha, walinzi wa Salaysa na wasaidizi wake waliingilia kati na kumwondoa mtu huyo kutoka jukwaani.

Wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii wamemkashifu Mbunge huyo kwa vitendo vyake.

TAGGED:
Share This Article