Mvua kubwa ambayo inashuhudiwa nchini Kenya, imesababisha kufurika kwa mbuga ya Maasai Mara baada ya mto Telek kuvunja kingo zake.
Mahoteli kadhaa ya watalii katika mbuga hiyo, yameathiriwa pakubwa na mafuriko hayo, huku shughuli za uokoaji zikiendelea.
Serikali ya kaunti ya Narok, imesema ushirikiano wake na serikali ya taifa pamoja na wanachama wa Mara Elephant, inatekeleza shughuli za uokoaji katika mbuga hiyo.
Katika taarifa kupitia mtandao wa X, shirika la msalaba mwekundi limesema kuwa takriban watu 90 kufikia sasa wameokolewa, huku kambi na mahoteli ya watalii yalioathiriwa yakifungwa.
Mafuriko hayo yamesomba daraja la mara pamoja na hema za watalii, baada ya mto huo kuvunja kingo zake Jumanne alasiri.
Pia kuna hofu kuwa huenda baadhi ya wanyama walisombwa na mafuriko hayo.