Mwanamuziki wa Tanzania Mbwana Yusuf Kilungi maarufu kama Mbosso Khan ametangaza kwamba amepona ugonjwa wa moyo ambao umekuwa ukimsibu.
Msanii huyo wa mtindo wa Bongo Fleva alitumia akaunti yake ya Instagram kutoa habari hizo nzuri.
Alifahamu kuhusu uhalisia wa kilichokuwa kikimsibu Disemba 28, 2024 pale aliposhiriki zoezi la kupima afya ya moyo katika hospitali ya magonjwa ya moyo ya Jakaya kikwete Jijini Dar Es Salaam.
Mbosso anasema madaktari walimwambia kwamba alizaliwa na tatizo hilo walilolitaja kuwa la umeme wa moyo huku wakiahidi kumsaidia apone kabisa.
Sasa juzi na jana anasema alikuwa na kipindi kigumu cha masaa 12 hadi 24 ambapo alikuwa na hofu kubwa lakini matokeo yake yamempa “Furaha na amani ya milele”.
Mbosso aliyeondoka kwenye kampuni ya Wasafi hivi maajuzi anasema alitibiwa na madaktari wajuzi wa masuala ya moyo kutoka Misri na kuruhusiwa kwenda nyumbani kwa mapumziko.
“Shukrani zangu nyingi za dhati zikufikie Popote Ulipo Mheshimiwa Rais wetu Tanzania Mama Yangu Samia Suluhu Hassan” aliandika Mbosso.
Aliendelea kusema kwamba juhudi za utawala wa Rais Samia zimewezesha upatikanaji wa matibabu ambayo aliambiwa awali yangepatikana tu nchini India.
Wengine aliowashukuru ni pamoja na katibu mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa BASATA Kedmon Mapana, mkurugenzi mkuu wa hospitali ya moyo ya Jakaya Kikwete Dkt. Peter Kisenge na wengine wengi.
“Asante Sana Mashabiki Zangu Wote Kwa Dua Zenu. Sasa nimepona na kazi inendelee.” alimalizia msanii huyo.