Uongozi mpya wa Chama cha Wahariri nchini (KEG), utajulikana leo Jumamosi wakati wahariri watakapopiga kura za kuwachagua viongozi wapya.
Wagombea wamekuwa wakitalii vyumba mbalimbali vya habari kutafuta uungwaji mkono.
Hafla ya upigaji kura itafanyika katika Chuo Kikuu cha Daystar kati ya saa tatu asubuhi na saa saba mchana.
Rais wa sasa wa KEG Zubeidah Kananu, kutoka kampuni ya Standard Media Group, anatafuta kutetea kiti chake na kuhudumu kwa muhula wa pili na mwisho baada ya kukamilika kwa muhula wake wa kwanza wa miaka miwili.
Hata hivyo, anakabailiwa na ushindani mkali kutoka kwa mwanahabari Yvonne Okwara kutoka kampuni ya Royal Media.
Wawili hao waliminyana katika mdahalo ulioandaliwa juzi Alhamisi jioni katika Chuo Kikuu cha Aga Khan.
Huku Kananu akitetea utendakazi wake kwa kipindi alichohudumu akitoa mfano wa ongezeko la mapato ya chama, Okwara alitilia shaka utendakazi wa chama hicho akisema kuna mengi yanayostahili kuboreshwa.
Kulingana naye, wahariri wengi bado hawajajiunga na chama kwani hawaoni manufaa ya kujiunga nacho.
KEG ina uanachama wa wahariri wapatao 300, na ada ya shilingi 7,000 wanayotozwa wahariri ili kujiunga inasemekana kuwa kikwazo kwa wengi.
Ni ada hiyo ambayo ni chanzo cha wahariri wapatao 135 pekee kupiga kura badala ya jumla ya wahariri 298 ambao ni wanachama wa KEG.
Ila, siyo urais wa KEG unaogombewa pekee.
Mhariri wa KBC Agnes Mwangangi na mwanahabari mkongwe wa zamani wa shirika hilo Toepista Nabusoba watatoana kijasho yamkini chembamba ili kubaini ni nani kati yao atahudumu kama mwanachama wa KEG akiwakilisha redio kwa kipindi cha miaka mwili ijayo.
Nabusoba anatafuta kuhudumu kwa muhula mwingine baada ya kumalizika kwa muhula wake wa kwanza.
Kunao wanachama watakaohudumu katika nyadhifa mbalimbali baada ya uteuzi wao kukosa wapinzani.
Wao ni Francis Openda atakayehudumu kama Naibu Rais wa KEG.
Naibu Mhariri Mkuu wa KBC Millicent Awuor atahudumu kwa kipindi cha pili kama mwanachama wa KEG akiwakilisha televisheni baada ya kukosa mpinzani. Awali, James Smart kutoka Nation Media Group alimezea mate wadhifa huo lakini akafungiwa nje kwa kukosa kutimiza vigezo vilivyowekwa.
Mwingine aliyekosa mpinzani ni Linda Bach na kwa misingi hiyo ana ridhaa ya kuhudumu kama mwanachama wa KEG akiwakilisha vyombo vya habari vya machapisho huku Kenfrey Kiberenge akiviwakilisha vyombo vya habari vya mtandaoni.
Hata hivyo, wanachama wa KEG wanatakiwa kuamua ni nani kati ya Nathan Nayere Masambu na Dkt. Julius Ombui Bosire atawakilisha wanazuoni chamani.
Martin Maasai, Ruth Nesoba na Mbugua Ng’ang’a watahudumu kama wadhamini wa KEG. Wote hao pia walipewa tiketi ya bwerere ya kuhudumu baada ya kukosa wapinzani.