Mbio za nyika za msururu wa AK kufanyika Kapsokwony

Marion Bosire
1 Min Read

Mkondo wa pili wa mbio za nyika za Msururu wa Kitaifa wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) unatarajiwa kufanyika Jumamosi, Oktoba 26, mjini Kapsokwony, huku wanariadha wakiahidiwa zawadi ya maelfu ya pesa.

Mashindano hayo yataandaliwa katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kapsokwony, Mt Elgon, yakihusisha mbio za U-20 kwa wanaume na wanawake, pamoja na mbio za wakubwa za kilomita 10 na mbio za mzunguko mmoja wa kilomita mbili kwa washiriki wote.

Wanariadha tajika wanatarajiwa kushiriki akiwemo Asbel Kiprop upande wa wanaume na Maureen Chepkoech kwa wanawake.

Mratibu wa hifadhidata mpya ya kidijitali ya wanariadha wa AK, Kennedy Tanui, ametangaza kuwa mfumo huo sasa unatumika kwa misururu yote ya kitaifa ya mbio za nyika. Amewahimiza wanariadha kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo za Kapsokwony.

“Nina furaha kutangaza kwamba mfumo wetu mpya wa usajili wa wanariadha – jukwaa la ubunifu linalorahisisha mchakato wa utoaji huduma kwa wanariadha wetu sasa unatumika na ulianza kutumika kwenye mkondo wa kwanza wa mbio za nyika huko Machakos, tunapoelekea mkondo wa pili mjini Kapsokwony,” Tanui alisema.

Hifadhidata hiyo mpya na zawadi ya hadi shilingi 50,000 ni sehemu ya mpango wa AK wa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya riadha nchini Kenya.

Share This Article