Waziri Mpya wa Fedha John Mbadi amechukua rasmi hatamu za uongozi wa wizara hiyo.
Mbadi alikabidhiwa mikoba ya wizara hiyo na mtangulizi wake Prof. Njuguna Ndung’u katika makao makuu ya wizara leo Jumatatu.
Prof. Ndung’u ni miongoni mwa angalau mawaziri 10 waliopigwa kalamu wakati Rais William Ruto alipovunja Baraza la zamani la Mawaziri.
Mbadi anachukua rasmi uongozi wa Wizara ya Fedha wakati wengi wakisubiri kuona namna atakavyokabiliana na ulipali wa deni kubwa la taifa ambalo kima chake ni karibu trilioni 10.
Aidha, wengi watafuatilia kwa makini kuona namna atakavyoongoza juhudi za ukusanyaji ushuru baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha 2024.
Mbadi ni miongoni mwa viongozi wa chama cha ODM walioteuliwa kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri.
Wengine ni Hassan Joho (Waziri wa Madini), Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama vya Ushirika) na Opiyo Wandayi (Waziri wa Nishati).