Mazungumzo yaangazie maslahi ya Wakenya, ashauri Asofu Sapit

Martin Mwanje
2 Min Read

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiangilikana humu nchini, ACK Jackson ole Sapit ametoa wito kwa timu za mazungumzo yanayolenga kuleta amani nchini kuyapa kipaumbele maslahi ya Wakenya na kuhakikisha mazungumzo hayo yanazaa matunda.

Timu za Kenya Kwanza na Azimio zinatarajiwa kuanza rasmi mazungumzo wiki ijayo baada ya kukutana juzi Jumatano na kukubaliana juu ya kanuni zitakazoongoza mazungumzo kati yao.

Askofu Sapit amesema katika mazungumzo yoyote yale, kuna maoni yanayotofautiana lakini amezitaka pande zote kulegeza kamba kwa manufaa ya taifa.

“Mazungumzo yaliyoanza juzi Jumatano yanatia moyo kwa sababu wanapokaa chini kuzungumza, nchi inakuwa na amani, na tunatoa wito kwao kukoma kuweka vizuizi kwenye mazungumzo hayo na kutishiana kwani wakifanya hivyo hawataenda mbali,” alishauri Askofu Sapit akiwa mjini Malindi.

Aliwahutubia wanahabari baada ya kuongoza hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa ofisi ya Parokia ya Kiangiliakana ya Langobaya.

Alitoa wito wa mazungumzo hayo kutoangazia maslahi ya wanasiasa bali masuala yanayowaathiri Wakenya ili kuwakwamua kutoka lindi la umaskini.

Kulingana naye, maslahi ya Wakenya hayawezi yakasuluhishwa kupitia vurugu na ubabe wa kisiasa, akiongeza kuwa taifa hili ni la Wakenya wote bila kujali miegemeo ya kisiasa.

Mjini Kakamega, viongozi wa Azimio wakiongozwa na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Ayub Savula pia waliunga mkono mazungumzo hayo wakiyataja kuwa suluhu ya kudumu kwa changamoto zinazolikumba taifa hili.

Mwakilishi wa Wanawake katika bunge la taifa Elsie Muhanda aliwataka viongozi husika kusalia macho na kuhakikisha suluhu ya kudumu inapatikana ili kuzuia umwagikaji damu kila baada ya uchaguzi.

Timu za Kenya Kwanza na Azimio zilikutana juzi Jumatano ili kuweka kanuni zitakazoongoza mazungumzo kati yao yanayotarajiwa kuanza rasmi wiki ijayo.

Kenya Kwanza inaongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah wakati kikosi cha Azimio kikiongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.

Carolyn Necheza na Emmanuel Masha wa KNA wamechangia taarifa hii. 

Website |  + posts
Share This Article