Wito wa Jaji Mkuu Martha Koome wa kutaka kufanya mazungumzo na Rais William Ruto kuhusiana na madai ya kukithiri kwa ufisadi katika idara ya mahakama unazidi kuibua maoni mbalimbali.
Upinzani ukiongozwa na kinara wa Azimio Raila Odinga tayari umepinga kufanyika kwa mazungumzo ya aina hiyo ukisema yataathiri utendakazi wa idara ya mahakama.
Msimamo sawia umechukuliwa na chama cha mawakili nchini, LSK ambacho kimemtaka Jaji Koome kutojiingiza katika mazungumzo ya aina hiyo.
Hata hivyo, akizungumza katika uwanja wa Mowlem katika eneo bunge la Endebess, kaunti ya Trans Nzoia leo Jumatano, Rais Ruto amewapuuzilia mbali viongozi wa upinzani wanaopinga kufanyika kwa mazungumzo kati ya serikali, idara ya mahakama na bunge.
Ameshangaa ni kwa nini viongozi wa upinzani wanapinga mazungumzo kati yake na viongozi wengine wa asasi huru ikiwa ni pamoja na idara ya mahakama, ilhali alifanya mazungumzo nao siku chache zilizopita.
Amesema mazungumzo kati ya mihimili mitatu ya serikali yanakusudia kuboresha vita dhidi ya ufisadi ambao umechelewesha maendeleo nchini.
“Wale wanaopinga mazungumzo kati ya taasisi mbalimbali ni wale ambao wamesajiliwa na wakora, matapeli na wahujumu, aibu kwao,” alisema Ruto.
“Yeyote ananayepinga viongozi kukutana kutafuta njia za kutatua matatizo hastahili kuongoza kamati ya josho la ng’ombe.”