Mawaziri wawili wateule kusailiwa Aprili 14

Tom Mathinji
1 Min Read
Mawaziri wawili wateule kusailiwa Aprili 14,2025.

Mawaziri wawili wateule Geoffrey Ruku wa Utumishi wa Umma na Hanna Chptumo wa Jinsia, watasailiwa na bunge Aprili 14,2025.

Wawili hao waliteuliwa mwezi uliopita, baada ya Rais William Ruto kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.

Kupitia kwa arifa kutoka kwa karani wa bunge la taifa  Samuel Njoroge, mchakato wa kuwasaili mawaziri hao utatekelezwa na kamati kuhusu uteuzi, ambayo inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa bunge.

Wawili hao wanatarajiwa kuwasilisha kwa kamati hiyo vyeti vya masomo, vyeti kutoka Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), Halmashauri ya Kukusanya Ushuru (KRA) na Bodi ya kutoa mikopo kwa Masomo ya Juu (HELB).

Vyeti vingine vinavyohitajika ni ile kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Msajili wa Vyama vya Kisiasa na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu.

Wakati huo huo karani huyo wa bunge alikaribisha maoni kutoka kwa umma kuhusu ufaafu wa wawili hao kufikia Aprili 10, 2025 saa kumi na moja jioni.

Website |  + posts
Share This Article