Mawaziri wateule kusailiwa hata wikendi

Marion Bosire
2 Min Read
Majengo ya bunge la Kenya.

Bunge la taifa limetoa ratiba ya kusaili walioteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu kama mawaziri katika baraza jipya la mawaziri.

Kulingana na ratiba hiyo, wateule hao watasailiwa hadi Jumamosi na Jumapili kwani usaili utafanyika kati ya Alhamisi Agosti Mosi na Jumapili Agosti 4 2024.

Siku ya kwanza wataohojiwa ni Kithure Kindiki ambaye amerejeshwa kwenye wizara ya usalama wa taifa, Daktari Debra Mlongo Barasa ambaye amependekezwa kuchukua mahala pa Susan Nakhumicha katika wizara ya Afya, Alice Wahome wa Ardhi, Julius Migosi wa Elimu na Soipan Tuya wa Ulinzi.

Ijumaa tarehe mbili Agosti itakuwa zamu ya Andrew Mwihia Karanja wa Kilimo, Aden Duale wa Mazingira, Eric Muriithi Muga wa maji, David Chirchir wa Barabara na uchukuzi na Margaret Nyambura Ndung’u wa mawasiliano na uchumi Dijitali.

John Mbadi wa fedha, Salim Mvurya wa biashara na uwekezaji, Rebecca Miano wa utalii, Opiyo Wandayi wa Nishati na Kipchumba Murkomen wa Vijana na Michezo watasailiwa Jumamosi.

Kundi la mwisho kusailiwa linajumuisha Hassan Joho wa madini, Alfred Mutua wa Leba na utunzi wa jamii, Ambetsa Oparanya wa Vyama vya ushirika, Justin Muturi wa utumishi wa umma na Stella Lang’at wa masuala ya Jinsia, utamaduni na sanaa.

Kamati ya bunge kuhusu uteuzi itatekeleza usaili huo kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni katika majengo ya bunge.

 

Website |  + posts
Share This Article