Wawakilishi wadi wa kaunti ya Bomet Ijumaa jioni, waliwatimua mawaziri watatu wa kaunti hiyo kwa madai ya utepetevu kazini.
Waziri wa Fedha Andrew Sigei, mwenzake wa barabara Erick Ngetich, yule wa utumishi wa umma Joseph Kirui, waliodolewa baada ya wawakilishi wadi kupiga kura na kufikisha idadi ya kura 19 zilizohitajika kuwatimua.
Wawakilishi wadi wote 28 waliohudhuria kikao hicho, walipiga kura kuwaondoa afisini mawaziri hao, huku wakisifia hatua hiyo kuwa itaimarisha uongozi katika serikali ya kaunti hiyo.
Walitoa wito kwa gavana wa kaunti hiyo Dkt. Hillary Barchok, kuchukua hatua za haraka na kuwaondoa afisini mawaziri hao, wakitaka uwajibishaji wa watumishi wa umma.
Spika wa bunge la kaunti ya Bomet Cosmas Korir, alipongeza hatua ya bunge hilo, akidokeza kuwa hiyo ni onyo kwa mawaziri wengine ambao wanatumia visivyo Mali ya umma.
Korir alisema hatua hiyo itaimarisha utoaji huduma na uwajibikaji kwa wananchi.