Kuambatana na agizo la Rais William Ruto kwamba mawaziri waongoze upanzi wa miti kila siku kwa muda wa miezi sita ijayo kuanzia leo Jumatatu Mei 13, 2024, ratiba ya wiki hii imetolewa.
Wizara ya Mazingira na misitu ndiyo imeandaa ratiba hiyo na leo ni zamu ya mwanasheria mkuu Justin Muturi ambaye ataongoza shughuli hiyo katika msitu wa milima ya Ngong kaunti ya Kajiado.
Kesho Jumanne Mei 14, 2024, waziri wa elimu Ezekiel Machogu atazuru kaunti ya Trans-Nzoia kwa sababu hiyo ambapo atapanda miche ya miti katika maeneo ya Sosio, Saboti, Kapolet na Saiwa.
Salim Mvurya waziri wa uchimbaji madini na uchumi wa baharini atafuatia siku ya Jumatano Mei 15, 2024 ambapo ataongoza shughuli ya kupanda miti katika maeneo ya Hirimana na Mwinai katika kaunti ya Tana River na maeneo ya Pandanguo na Lake Kenyatta katika kaunti ya Lamu.
Alhamisi Mei 16, 2024 waziri wa utalii Alfred Mutua atakuwa katika kaunti za Kitui na Taita Taveta hususan maeneo ya Muumoni, Itikoni na Lake Jipe kwa sababu hiyo.
Waziri wa kawi Davis Chirchir atafunga wiki ya kwanza ya shughuli hiyo ya mawaziri kuongoza upanzi wa miche ya miti ambapo atazuru kaunti za Kericho na Baringo.
Rais William Ruto alitoa maelekezo hayo Ijumaa Mei 10, 2024 wakati wa shughuli ya kitaifa ya upanzi wa miche ya miti.