Mawaziri wa Ulinzi wa EAC wapendekeza muda wa kikosi chake DRC uongezwe

Marion Bosire
2 Min Read

Mawaziri wa Ulinzi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC walikongamana jijini Arusha nchini Tanzania na mojawapo ya masuala ambayo yalijadiliwa ni hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC. 

Kulingana na Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale, mawaziri hao walipendekeza kuongezwa kwa muda wa kuhudumu wa kikosi cha EACRF katika eneo hilo la mashariki ya DRC.

Kikosi hicho kiliongezewa muda tena mwezi Septemba katika kikao cha 22 cha viongozi wa nchi wanachama wa EAC kilichofanyika jijini Nairobi.

“Kwa kuangazia mazuri ambayo kikosi cha EACRF kimeafikia nchini DRC, kikao cha Mawaziri wa Ulinzi kilipendekeza kwamba muda wa kikosi hicho uongezwe hadi pale ambapo amani na uthabiti utaafikiwa huko,” alisema Duale kwenye taarifa.

Alisema Kenya ambayo ni moja kati ya nchi ambazo zimechangia wanajeshi wa kikosi cha EACRF, inakubali pendekezo hilo na inajitolea kuunga mkono juhudi za kutafuta amani na maendeleo ya kiuchumi ya DRC.

Kulingana na Duale, mawaziri hao aidha walijadili masuala mengine mengi yanayohusu kanda hii wakiwa pamoja na wataalamu wa sheria na usalama.

Alikuwa ameandamana na Naibu Mkuu wa Majeshi ya Kenya Luteni Jenerali Jonah Mwangi, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha EACRF Meja Jenerali Alphaxard Kiugu, Mkuu wa Mipango katika makao makuu ya ulinzi nchini Brigedia Kimonge na Kanali Ngatia ambaye ni msimamizi wa masuala ya sheria katika jeshi la Kenya.

Mawaziri waliohuudhuria kikao hicho ni Alain Tribert Mutabazi wa Burundi ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la Mawaziri wa Ulinzi wa EAC, Dkt. Stergomena Lawrence wa Tanzania, Vincent Ssempijja wa Uganda, Jean-Pierre Bemba wa DRC na mwakilishi wa Sudan Kusini.

Share This Article