Mawakili leo Ijumaa wameandamana hadi nje ya Mahakama ya Juu kulalamikia tuhuma zinazoendelezwa dhidi ya idara ya mahakama.
Wakiongozwa na chama chao cha LSK chini ya uenyekiti wa Eric Theuri, mawakili hao wameikosoa serikali kwa kuendelea kuishambulia idara ya mahakama na kutaka iheshimiwe.
Wakati wa maandamano hayo, walibeba mabango yanayotoa wito wa kuheshimiwa kwa idara hiyo.
Rais William Ruto ameishutumu idara ya mahakama kwa kula njama na watu fulani kuhujumu utekelezwaji wa miradi ya serikali.
Anatoa mfano wa kesi zilizowasilishwa dhidi ya mpango wa nyumba za bei nafuu na upatikanaji wa afya kwa wote.
Hata hivyo, mawakili hao wanasema idaya ya mahakama inapaswa kulindwa kama ilivyoelezwa katika katiba ya mwaka 2010 kwani idara hiyo ni nguzo muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka.
Wanasiasa kadhaa wa upinzani akiwemo kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa ni miongoni mwa viongozi walioshiriki maandamano ya hii leo Ijumaa.