Waziri wa Usalama wa Taifa Prof. Kithure Kindiki amewaomba Wakenya msamaha kutokana na mauaji yaliyotokea katika msitu wa Shakahola katika kaunti ya Kilifi.
Jumla ya watu 351 wamethibitishwa kufariki katika msitu huo huku awamu ya nne ya kufukua miili ikirejelewa jana Jumatatu ambapo miili 12 ilifukuliwa. Mtu mmoja alifariki akiwa hospitalini.
Waathiriwa wanaaminika kuwa wafuasi wa dhehebu la Good News International linaloongozwa na mhubiri Paul Mackenzie.
Mackenzie kwa sasa anazuiliwa na maafisa wa polisi huku uchunguzi mkali ukiendelea kuhusiana na kisa hicho.
“Naomba msamaha kwa watu wa Kenya kwamba hili halikupaswa kutokea,” alisema Waziri Kindiki leo Jumanne alipofika mbele ya kamati ya bunge la Seneti inayochunguza mauaji hayo leo Jumanne. Kamati hiyo inaongozwa na Seneta wa Tana River Danson Mungatana.
“Huu ndio ukiukaji mbaya zaidi wa usalama ambao nchi yetu imewahi kushuhudia.”
Ili kuepusha kutokea kwa mauaji kama hayo, Prof. Kindiki alisema serikali inashinikiza kutekelezwa kwa marekebisho ya kisheria ili kukabiliana na wahubiri walaghai wanaotumia vibaya Injili kuwapotosha wafuasi wao.
Prof. Kindiki aliwaelezea Maseneta kuwa ameaiagiza Idara ya Mashtaka ya Umma kuhakikisha inakusanya ushahidi wa kutosha utakaowezesha kuwajibishwa kwa wale wote waliohusika katika mauaji hayo ambayo yamegonga vichwa vya habari kitaifa na kimataifa.
“Yeyote atakayechangia kutowajibishwa kwa wahusika wa mauaji hayo hatasamehewa,” alionya Kindiki.
Huku uchunguzi ukiendelea kubaini mmiliki wa msitu wa Shakahola palipotokea mauaji hayo, Waziri huyo alisema Mackenzie alikuwa na udhibiti wa msitu huo kufikia wakati wa mauaji hayo.
kulingana naye, upande wa mashtaka unakusanya ushahidi kuhusiana na umiliki shamba hilo na mbivu na mbichi itajulikana punde suala hilo litakapowasilishwa mahakamani.