Mauaji ya mwanafunzi wa kike yazua maandamano kote nchini Italia

Marion Bosire
2 Min Read

Watu wengi wamejitokeza kushiriki maandamano kwenye barabara za miji kadhaa nchini Italia kulalamikia mauaji ya mwanafunzi wa kike.

Maandamano makubwa yalishuhudiwa katika miji ya Roma, Milan na mingine kuunga mkono siku ya kimataifa ya kumaliza dhuluma dhidi ya wanawake.

Maandamano hayo yalichochewa na mauaji ya mwanadada wa umri wa miaka 22 mwanafunzi wa chuo kikuu aliyekuwa anakaribia kufuzu.

Giulia Cecchettin, wa eneo la Venice aliuawa na aliyekuwa mpenzi wake siku chache kabla ya siku ya mahafali.

Jumamosi jamaa huyo alirejeshwa nchini Italia kutoka Ujerumani ambako alikuwa amekimbilia baada ya kutekeleza mauaji hayo.

Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni, ambaye ndiye wa kwanza wa kike katika wadhifa huo, alihakikishia wanawake wa Italia uungwaji mkono kupitia mtandao wa Facebook.

Mauaji ya wanawake yamekuwa donda sugu nchini Italia na kulingana na takwimu, wanawake 106 waliuawa nchini humo mwaka 2022, ongezeko kutoka wanawake 104 waliouawa mwaka 2021.

Wanawake zaidi ya elfu 3 huuawa kila mwaka kote barani Ulaya kila mwaka ukatili unaotekelezwa na wapenzi wao au na watu wa familia zao, haya ni kwa mujibu wa tume ya Ulaya.

Msimamizi wa mambo ya nje katika umoja wa Ulaya Josep Borrell anasema kwamba haki za wanawake na wasichana zimekuwa zikikiukwa au kutupiliwa mbali kabisa ulimwenguni kote, hatua inayolemaza maendeleo yaliyoafikiwa katika muda wa miaka kadhaa.

Rais wa umoja huo Ursula von der Leyen kupitia mtandao wa X amependekeza kubuniwa kwa sheria ya kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake.

Share This Article