Jaji Grace Nzioka ambaye pia ni Jaji Msimamizi wa Mahakama ya Naivasha kwa sasa anasoma hukumu katika kesi inayowakabili mwanahabari Jackie Maribe na mpenzi wake wa zamani Joshua Irungu, maarufu kama Jowie.
Maribe na Jowie wanakabiliwa na mashtaka ya kumuua mfanyabiashara Monicah Kimani mnamo mwezi Septemba mwaka wa 2018.
Hukumu dhidi yao ilikuwa imepangwa kutolewa Machi 15, 2024 lakini timu za wanasheria katika kesi hiyo zikakubaliana kuiratibu upya ili itolewe leo Ijumaa.
Maribe na Jowie wanashukiwa kuhusika katika mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani mnamo mwaka 2018, mashtaka ambayo wameyakanusha.
Jowie ndiye mshukiwa mkuu huku Maribe akishtakiwa kwa kuwa msaidizi katika mauaji hayo.
Mashahidi 35 walitoa ushahidi wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Marehemu Kimani alipatikana ameuawa katika makao yake ya Lamuria Gardens, karibu na barabara ya Dennis Pritt mwaka 2018 mtaani Kilimani.
Tutakuletea hukumu itakayotolewa dhidi ya washukiwa na Jaji Nzioka punde atakapomaliza kuisoma.