Mauaji ya MCA wa Dela: LSK yataka uchunguzi wa haraka kufanywa

Martin Mwanje
1 Min Read
Yussuf Hussein Ahmed - MCA wa Dela aliyeuawa

Chama cha Wanasheria nchini, LSK sasa kinatoa wito wa kufanywa kwa uchunguzi huru na wa kina haraka iwezekanavyo kuhusiana na mauaji ya Mwakilishi Wadi ya Dela katika kaunti ya Wajir, Yussuf Hussein Ahmed.

Ahmed alipatikana ameuwa baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana Ijumaa, Septemba 13, 2024 majira ya saa mbili usiku kwenye barabara ya Enterprise jijini Nairobi.

Baada ya siku nyingi za mahangaiko na kumtafuta mpendwa wao, familia yake ilithibitisha mauaji yake baada mwili wake kupatikana katika Ziwa Yahud.

“Kuuawa kwake ni ukiukaji mkubwa wa haki zake za msingi, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi kama ilivyoelezwa kwenye Kifungu cha 26(1) cha Katiba ya Kenya (2010),” amesema Faith Odhiambo, Rais wa LSK.

“LSK inalaani vikali mauaji yasiyokubaliwa kisheria, ambayo siyo tu kwamba yanakiuka utawala wa sheria lakini pia yanatia hofu na ukosefu wa usalama kwa umma.”

Chama hicho sasa kinamtaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga kumuelekeza Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kufanya uchunguzi wa dharura kwa lengo la kuwakamata na kuwashtaki waliohusika katika mauaji hayo.

 

TAGGED:
Share This Article