‘Mauaji ya kiongozi wa Hamas sio mashambulizi dhidi ya Lebanon’ – Israel

Martin Mwanje
2 Min Read

Israel imesisitiza kuwa mauaji ya kiongozi wa Hamas huko Beirut hayakuwa mashambulizi dhidi ya Lebanon, licha ya maadui zake kutoa onyo la kulipaza kisasi kwa mauaji hayo.

Msemaji wa serikali ya Israel, alisema, ”Saleh al-Arouri alifariki katika shambulio dhidi ya Hamas.”

Hamas imelaani mauaji hayo, huku mshirika wake Hezbollah ikisema ni shambulio dhidi ya mamlaka ya Lebanon.

Wakati huohuo Waziri Mkuu wa Lebanon, aliishutumu Israel kwa kujaribu “kuiingiza Lebanon katika mvutano.”

Vyombo vya habari vya Lebanon vinaripoti kwamba Arouri, naibu kiongozi wa kisiasa wa Hamas, aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani kusini mwa Beirut pamoja na watu wengine sita – makamanda wawili wa kijeshi wa Hamas na wanachama wengine wanne.

Alikuwa kiongozi muhimu katika Brigedi za Qassam, mrengo wenye silaha wa Hamas, na mshirika wa karibu wa Ismail Haniyeh, kiongozi wa Hamas.

Alikuwa Lebanon kwa ajili ya uhusiano kati ya kundi lake na Hezbollah.

Msemaji wa Israel Mark Regev hakutaka kuthibitisha kuwa Israel ilifanya mauaji hayo, msimamo wa kawaida kwa maafisa wa Israel, lakini aliiambia MSNBC: “Yeyote aliyefanya hivyo, ni lazima ieleweke kwamba hili halikuwa shambulio dhidi ya taifa la Lebanon. Yeyote aliyefanya hivi ana uadui na Hamas. Hilo liko wazi kabisa.”

Arouri mwenye umri wa miaka 57, ndiye kiongozi mkuu zaidi wa Hamas kuuawa tangu Israel ilipoingia vitani na kundi hilo baada ya shambulio la Oktoba 7.

Siku hiyo, wapiganaji wa Hamas walivamia Israeli na kushambulia jamii zilizo karibu na mpaka, na kuua watu wapatao 1,200, wengi wao wakiwa raia, na kuwachukua karibu watu 240 hadi Gaza kama mateka.

Share This Article