Matiang’i ateuliwa naibu kiongozi wa chama cha Jubilee

Marion Bosire
2 Min Read

Fred Matiang’i ambaye ni waziri wa zamani wa usalama wa ndani, ameteuliwa kuwa naibu kiongozi wa chama cha Jubilee.

Haya yamefanyika leo Oktoba 30, 2025 wakati wa mkutano wa baraza kuu la kitaifa la chama hicho, mkutano ambao pia ulimuunga mkono kama mwaniaji Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Katibu mkuu wachama hicho Jeremiah Kioni aliwahi kutangaza awali kwamba chama hicho tayari kimeamua kumuunga mkono Matiang’i katika kinyang’anyiro hicho.

Yapata miezi minane iliyopita, Kioni katika mahojiano na runinga moja humu nchini, alisema anamuunga mkono Matiang’i kuwa mwaniaji Urais wa chama hicho lakini akafafanua kwamba walikuwa wakijadiliana na wanachama.

Mkutano wa leo ulikuwa chini ya uenyekiti wa kiongozi wa chama hicho Uhuru Kenyatta na ilifafanuliwa kwamba Matiang’i atawakilisha chama cha Jubilee katika muungano wa upinzani.

Katika majukumu hayo, Matiang’i atasaidiwa na mwenyekiti wa chama  Saitoti Torome, huku chama hicho kikisisitiza kwamba bado kimejitolea kikamilifu kwa muungano wa upinzani.

Matiang’i aliwasilisha ombi la kuwa mwaniaji Urais wa chama cha Jubilee kwa baraza hilo la kitaifa, ombi ambalo liliungwa mkono na wanachama wa baraza hilo.

Uamuzi mwingine uliofanywa kwenye mkutano huo ni wa kuhuisha na kukitia nguvu chama hicho kupitia usajili wa wanachama wapya kote nchini.

Hatua hiyo inatarajiwa kujenga upya mtandao wa chama hicho mashinani na kurejesha imani ya umma.

Website |  + posts
Share This Article