Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Amin Mohamed hatimaye wamefika mahakamani kuhusiana na utekaji nyara wa wanaume watatu katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos.
Juhudi za mahakama kuwataka wawili hao kufika mahakamani awali ziligonga mwamba, wakati wote ho wakituma wanasheria wao kuwawakilisha.
Leo Alhamisi, hali ya usalama ilikuwa imeimarishwa katika majengo ya mahakama wakati wawili hao wakifika mbele ya Jaji Chacha Mwita ili kumulika mwanga juu ya hatima ya wanaume hao watatu waliotekwa nyara mwezi Disemba mwaka jana.
Familia za wanaume hao zimekuwa zkitoa wito kwa serikali kuzisaidia kubaini walipo wapendwa wao.
Kanja amekanusha madai ya kuhusika kwa maafisa wa polisi katika visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara nchini.
Ameongeza kuwa Huduma ya Taifa ya Polisi anayoiongoza imeimarisha uchunguzi kubaini waliko watu waliotekwa nyara nchini.
Kulingana na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNCHR, watu wasiopungua 20 wametekwa nyara nchini tangu mwezi Juni mwaka jana.