Mateka 4 zaidi wa Israel wafariki Gaza

Tom Mathinji
1 Min Read

Jeshi la Israel linasema kuwa limethibitisha vifo vya watu wanne zaidi waliotekwa nyara na Hamas  Oktoba 7,2023.

Linasema wanne hao waliuawa wakiwa pamoja wakati wa operesheni ya Israel huko Khan Younis kusini mwa Gaza, na kuongeza kuwa miili yao ingali inashikiliwa na wanamgambo hao.

Wanaume hao walitajwa kuwa ni Muingereza-Muiisrael Nadav Popplewell, 51, Chaim Peri, 79, Yoram Metzger, 80, na Amiram Cooper, 85.

Msemaji wa IDF Adm Daniel Hagari alisema taarifa za kijasusi zilizokusanywa katika wiki za hivi majuzi zimehitimisha tathmini hiyo.

“Tunatathmini kuwa wanne hao waliuawa wakiwa pamoja katika eneo la Khan Younis wakati wa operesheni yetu huko dhidi ya Hamas,” alisema bila kutoa maelezo zaidi.

Mwezi uliopita, Hamas ilidai kuwa Nadav Popplewell alifariki dunia katika shambulizi la Israel mnamo mwezi Aprili. Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema inachunguza, lakini hakuna uthibitisho wa kifo chake hadi sasa.

Hamas ilitoa video inayowaonyesha wanaume wengine watatu mwezi Desemba.

TAGGED:
Share This Article