Matayarisho ya sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu kufariki kwa mwanzilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kesho yamekamilika.
Maadhimisho hayo yataandaliwa nyumbani kwake Wilayani Butiama eneo la mara kesho Jumatatu, Oktoba 14.
Wakazi zaidi ya 500 kutoka Afrika Mashariki wamekongamana Butiama kwa hafla hiyo, ambayo pia itashuhudiwa kutawazwa kwa marehemu Nyerere kuwa mtakatifu.
Shirika la Afrika Mashariki Fest lenye makao yake nchini Uganda limeandaa sherehe hizo ambapo zaidi ya watu 500 kutoka Uganda na Kenya pamoja na wenyeji wamewasili tayari kuzihudhuria.
Afisa Mkuu Mtendaji ww Afrika Mashariki Fest Ronex Kisembo Tendo amewataka wana Afrika Mashariki kupitia kwa viongozi wao kukumbatia wito wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyoanzishwa na hayati Nyerere.
Kuhusu ratiba ya kesho, Kisembo anasema kuwa watafungua kwa ibada ya kanisa eneo la Butiama kabla ya mahujaji kuzuru nyumbani kwa marehemu Nyerere.
Viongozi mbalimbali kutoka EAC wanatarajiwa kuhudhuria wakiwemo Miriam Obote, mkewe Rais mwanzilishi wa Uganda Milton Obote, Mama Ngina Kenyatta, mkewe Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta na mkewe marehemu Nyerere, Maria.
Kisembo amesema pia wanapanga kuwasilisha makubaliano ya Butiama kuhusu vijana yatakayowashinikiza viongozi wa kuyasaini.
“Baada ya sherehe, sisi pia kama vijana tunapanga kuwasilisha makubaliano ya Butiama kwa viongozi wetu wa Afrika Mashariki kuyasaini ili tujue mustakabali wetu,” amesema Kisembo.
Marehemu Nyerere alizaliwa April 13 mwaka 1922 eneo na Butiama na alikuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika kati ya Oktoba 29 mwaka 1962 hadi Novemba 5, 1985 alipojiuzulu.