Matamshi ya Rais kuhusu mahakama yazidi kukosolewa

Marion Bosire
2 Min Read
Rais William Ruto.

Rais William Ruto alilalamika kuhusu idara ya mahakama akisema inatumiwa kuhujumu serikali matamshi ambayo yanaendelea kukosolewa.

Wa hivi punde zaidi kumkosoa Rais ni kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye amesema kwamba Rais William Ruto amevuka mpaka kutokana na shutuma hizo dhidi ya idara ya mahakama.

Kupitia taarifa Raila alisema kwamba alidhania serikali ya Kenya Kwanza ingeanza mwaka 2024 kwa namna tofauti hasa baada ya hatua zake kadhaa kusababishia wakenya machungu mwaka jana.

Anasema hilo halijadhihirika ila badala yake kiongozi wa nchi ametokea kuwa mkali zaidi ambapo aliamua kufokea idara ya mahakama kwa madai ya kuhujumu mipango ya serikali.

Raila anahimiza kiongozi wa nchi kutii mahakama akitaja hatua ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kutii uamuzi wa mahakama kuhusu uchaguzi wa Urais mwaka 2022 hata ingawa hawakukubaliana nao.

Alisema walikubali kwa sababu wanaelewa fika kwamba kutotii mahakama huenda kukachochea vurugu na kusababisha kuangamia kwa taifa.

Tume ya idara ya mahakama JSC kwa upande wake imesema imetambua shutuma dhidi ya majaji wa mahakama ambao walitoa maagizo yanayochukuliwa kuwa dhidi ya serikali.

JSC imehimiza majaji na maafisa wengine wa mahakama kuendelea kutoa huduma zao kwa mujibu wa sheria ikisema kwamba idara ya mahakama ni huru na ni mshirika sawa katika serikali.

Taarifa hiyo imetiwa saini na jaji mkuu Martha Koome ambaye pia ni mwenyekiti wa tume ya idara ya mahakama ambaye amehakikishia wakenya kwamba iwapo jaji fulani wamekwenda kinyume cha sheria atachukuliwa hatua stahiki.

Share This Article