Matamshi ya kejeli yamponza kocha wa timu ya wanawake ya Rwanda

Francis Ngala
2 Min Read
Kocha wa timu ya wanawake ya Rwanda Grace Nyinawumuntu: Photo/Courtesy

Kocha wa timu ya wanawake ya Rwanda Grace Nyinawumuntu amesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana na shirikisho la soka nchini humo kufuatia matamshi ya dharau aliyosema dhidi ya wachezaji wa timu ya Ghana.

Taarifa ya Shirikisho FERWAFA kwa umma ilithibitisha kumsimamisha kocha huyo kazi ‘kwa kipindi kisichojulikana’ kutokana na matamshi aliyotumia baada ya mchezo kati ya Rwanda na Ghana.

“Matamshi ya kocha wa timu ya taifa ya wanawake (Grace Nyinawumuntu) kuhusu wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Ghana yanakiuka kanuni na maadili ya soka la Rwanda.’ Taarifa ya shirikisho ilisema.

Adhabu ya shirikisho la soka nchini Rwanda ina ujio wa siku mbili baada ya timu ya wanawake ya Ghana (Ghana Black Queens) kudhalilisha wenyeji Rwanda kwa mabao saba bila jawabu 7-0, katika mchezo wa kufuzu kombe la Africa kwa akina dada, ambapo kocha huyo alisema kwamba wachezaji wa kike wa Ghana wanakaa kama wanaume.

Akiongea na wanahabari Nyinawumuntu alisema kuwa timu yake ilitishwa na hali ya kimwili ya wachezaji wa Ghana, ” Wana wasichana ambao wana homoni za kiume,” alisema Kocha huyo.

“Ni wasichana ambao wanakaa kama wanaume, timu yetu iliingiwa hofu ilipofika uwanjanai, tulishindwa kwasababu tulikuwa na hofu.” Nyinawumuntu aliongeza.

Timu ya wanawake ya Rwanda sasa itasafiri kuelekea Accra bila kocha mkuu kwa mchezo wa raundi ya pili huku Ghana Black Queens wakitumaini watavuna magoli ya kuipa ushindi zaidi katika uwanja wa nyumbani.

 

 

Website |  + posts

I am Versatile Multimedia Journalist with years of experience in Digital platforms, Live TV and Radio. In another world am a News Anchor and Reporter.

Share This Article