Rais William amesema bara la Afrika halitafuti tu ufadhili, lakini pia linataka ufadhili dhabiti kwa maendeleo ya bara hili.
Akizungumza leo Jumatatu wakati wa ufunguzi wa kongamano la shirika la kimataifa la maendeleo IDA21 katika jumba la mikutano ya kimataifa KICC Jiji Nairobi, kiongozi wa taifa alipendekeza kuwe na na mpango makhususi pamoja na mataifa kujitolea, ili kuhakikisha maisha bora kwa wote.
Alisema kongamano la IDA 21, limeandaliwa huku bara hili likikumbwa na changamoto kadhaa za kimataifa.
Rais Ruto alisema bara hili linakumbwa na mzozo wa kimaendeleo na madeni unaotishia uthabiti wa kiuchumi.
“Mataifa ya Afrika yanakabiliwa na mizozo ya maendeleo na madeni ambayo inaathiri udhabiti wa kiuchumi na dharura za hali ya anga ambazo zinahitaji kushughulikiwa,” alisema rais Ruto.
Alitoa wito kwa mataifa tajiri, kuongeza mchango wao kwa shirika la kimataifa la maendeleo IDA, kufika angalau dola bilioni 120.
“Tunatoa wito kwa washirika wetu….kuongeza mchango wao kwa IDA..hadi dola bilioni 120,” alisema Rais Ruto.
IDA hutoa mkopo wa riba nafuu kwa nchi 75 zinazoendelea kote duniani, huku benki ya dunia ikisema nusu ya nchi hizo zinatoka bara Afrika.
Fedha hizo hutumiwa na serikali kupiga jeki sekta za kawi, afya, uwekezaji katika kilimo na ujenzi wa miundomsingi.
Marais 16 wa Afrika pamoja na rais wa benki ya dunia Ajay Banga, walihudhuria kongamano hilo.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa pamoja na serikali ya Kenya na benki ya dunia.