Matabibu wamesitisha mgomo wa kitaifa uliodumu kwa kipindi cha miezi mitatu, baada ya kuafikiana na Magavana kuhusu matakwa yao leo Jumatatu.
Kwenye taarifa ya pamoja kwa wanahabari baina ya Baraza la Magavana nchini (CoG), na muungano wa matabibu nchini yaani Kenya Union of Clinical Officers (KUCO), mgomo huo umesitishwa baada ya zote pande mbili kuafikiana.
Maafikiano kati ya CoG na KUCO yanajumuisha;
- Kuanzishwa kwa majadiliano kuhusu nyongeza mpya ya mshahara kati ya CoG na KUCO, na kukamilishwa na kusainiwa katika muda wa siku 60.
2. Serikali za kaunti ambazo hazijawapandisha vyeo matabibu kufanya hivyo kufikia Septemba mosi mwaka huu.
3. Serikali za kaunti kuwaajiri maafisa wa afya zaidi kujaza nafasi zilizopo.
4. Hazina kuu kutenga bajeti kwa watoa huduma ya afya kwa wote (UHC), na wale wanaowashughulika wagonjwa wa Covid-19.
5. Matababibu wa hospitali za kaunti kupewa bima ya matibabu kuanzia Septemba mosi mwaka huu, kama wenzao wa hospitali za umma.
6. CoG na KUCO kushauriana na kaunti husika ili kubaini hatima ya malimbikizi ya mishahara ya miezi mitatu kwa wakati ambao matabibu wamekuwa kwenye mgomo.
7. Kusawazisha masharti ya kazi na mafao kwa matabibu wanaohudumu katika hospitali za umma na zile za kaunti.
8. Matabibu ambao wamekuwa kwenye mgomo tangu Machi 25 waripoti kazini ndani ya saa 24.
9. Matabibu wote ambao wamekuwa kwenye mgomo kutoadhibiwa.
Huduma katika hospitali za kaunti zilimelemazwa katika muda ambao matabibu hao wamekuwa kwenye mgomo.