Mashindano maalum ya Karate yaandaliwa Kakamega

Carolyn Necheza
1 Min Read

Shirikisho la Mchezo wa Karate, kaunti ya Kakamega liliandaa mashindano maalum mjini Kakamega kwa lengo la kuwachagua wachezaji watakaojiunga na wenzao kutoka kaunti zingine kule Nakuru. 

Timu hiyo itawakilisha Kenya katika michuano ya Afrika itakayofanyika jijini Abuja, Nigeria, na hatimaye kushiriki mashindano ya dunia yatakayoandaliwa jijini Cairo, Misri mwezi Juni mwaka huu.

Rais wa shirikisho hilo, Richard Mbinga, ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa zinazokumba mchezo huo nchini ni uhaba wa vifaa pamoja na sehemu za kufanyia mazoezi.

Ameitaka Wizara ya Elimu na ile ya Michezo kuruhusu michezo hiyo shuleni na kuweka vifaa pamoja na viwanja vya mazoezi katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu.

Kwa upande wake, Msaidizi Mkurugenzi wa Karate nchini, Stephen Wesonga, amesema kuwa suala la matumizi ya dawa za kusisimua misuli miongoni mwa wanamichezo limezingatiwa kwa makini akieeleza kuwa kuna vitengo maalum vinavyotoa ushauri kwa wachezaji na pia kufanya vipimo ili kubaini wale wanaoweza kudanganywa kutumia dawa hizo.

Naye Christopher Ouma, msimamizi wa mchezo huo katika kaunti ya Kakamega, ameeleza masikitiko yake kuhusu uhaba wa vifaa vya mchezo huo kwa watoto na hata watu wazima wanaoshiriki.

Carolyn Necheza
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *