Mashabiki wa timu inayoshiriki ligi kuu nchini Uingereza Manchester United kote nchini Kenya wamepanga shughuli ya utoaji damu katika maeneo mbali mbali wikendi ijayo.
Mpango huo utaongozwa na mashabiki wa matawi mbali mbali ya chama chao na unalenga kuhakikisha uwepo wa damu ya kutosha katika hifadhi za humu nchini ili kusaidia wagonjwa.
Februari 15 2025, mashabiki hao wataongoza utoaji damu ifuatavyo, wale wa tawi la Nairobi watatoa damu katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta -KNH, Wa Eldoret watatolea kwenye Potter’s House Academy na wa Mombasa watakutana kwenye hospitali ya Mombasa.
Uwanja wa maegesho ya magari wa benki ya Standard utatumiwa na mashabiki wa Manchester United wa Nakuru, wa Naivasha wakutane kwenye bustani ya manispaa ya Naivasha huku wale wa eneo zima la Gusii wakifanya hivyo kwenye uwanja wa hifadhi ya damu ya Kisii.
Mashabiki wa Ol Kalau watatoa damu katika maegesho ya magari ya mjini Ol Kalau karibu na afisi ya mkuu wa wilaya, wa Bungoma wakutane katika hospitali ya rufaa ya Bungoma na wa Turkana watoe damu katika hospitali ya rufaa ya Lodwar.
Wanachama wa tawi la magharibi watakutana katika uwanja wa chuo kikuu cha Kaimosi siku hiyo huku shughuli hiyo ikiahirishwa hadi mwezi Mei katika matawi ya
Meru, Tharaka Nithi, Isiolo na Nanyuki.
Mashabiki wote wa timu ya Manchester United kote nchini Kenya wanahimizwa kushiriki shughuli hiyo ya kuchangisha damu na kuleta mabadiliko.