Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Gilbert Masengeli amekanusha madai kuwa walinzi Jaji Lawrence Mugambi wameondolewa.
Ametaja madai hayo yaliyotolewa na Tume ya Huduma za Majaji (JSC) kuwa yenye nia mbaya.
Maafisa wawili wa ulinzi wa Jaji Mugambi wameondolewa siku chache baada ya Jaji huyo kutoa uamuzi wa kumtaka Masengeli akamatwe kwa kuidharau mahakama.
JSC imetaja hatua hiyo kuwa yenye nia ya kumtisha Jaji Mugambi kufuatia uamuzi wake wa kumtaka Masengeli akamatwe kwa kuidharau mahakama.
Madai ambayo yamemfanya Masengeli kujitetea vikali.
“Katika kisa cha Jaji Mugambi, maafisa hao wawili wa usalama ni maafisa kutoka huduma ya kawaida na kwa hivyo waliondolewa ili kushiriki mafunzo ya usalama wa viongozi mashuhuri, na mahali pao palichukuliwa na maafisa wa ulinzi wa viongozi mashuhuri kutoka kitengo cha polisi wa idara ya mahakama,” alisema Masengeli katika taarifa.
“Wajibu wa Inspekta Jenerali wa kulinda nchi ni mkubwa zaidi na kazi ya polisi ni ya kipekee. Ni wazi kwa umma kuwa wakati IG alipotakiwa kufika mbele ya mahakama, alikuwa anatathmini hali ya usalama katika maeneo ya Pwani na Kaskazini Mashariki. Kwa kutii agizo la mahakama, IG aliwakilishwa na Naibu IG wa Huduma ya Polisi nchini kwa sababu suala lililozungumziwa halikumhusu IG binafsi.”
Masengeli ametakiwa mara kadhaa kufika mbele ya mahakama kuelezea waliko wanaharakati watatu wanaodaiwa kukamatwa na polisi karibu mwezi mmoja uliopita.
Hata hivyo, amekaidi agizo la kufika mahakamani, hali ambayo ilimlazimu Jaji Mugambi kutoa uamuzi wa kukamatwa kwake kwa kuidharau mahakama.