Maseneta wamwandama Sakaja, Magavana wengine 29

Magavana hao wametakiwa kufika mbele ya kamati ya seneti kujibu maswali ya ukaguzi wa matumizi ya fedha ya mwaka 2024/2025.

radiotaifa
2 Min Read
Wanachama wa Kamati ya Kaunti ya Uhasibu wa Fedha za Umma ya Seneti wakati wa kikao

Taarifa ya Martin Mwanje na Abdiaziz Hashim

Kamati ya Kaunti ya Uhasibu wa Fedha za Umma ya Seneti imemtoza Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja faini ya shilingi nusu milioni.

Kamati hiyo pia imemwagiza Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kumwasilisha Gavana huyo mbele yake Jumatatu ijayo.

Hii ni baada ya Sakaja kususia kufika mbele ya kamati hiyo mara nne.

Kadhalika, kamati hiyo imesema ikiwa Gavana huyo hatafika mbele yake kujibu maswali, basi itaazimia kwamba Sakaja hapaswi kuhudumu katika wadhifa wa umma.

Ni azimio ambalo Maseneta wanasema wataliwasilisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC kwa lengo la kupisha mchakato wa kumtimua madarakani.

Sakaja anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo kujibu masuali kuhusiana na ukaguzi wa matumizi ya fedha ya mwaka 2024/2025, maswali yanayohusisha mpango wa Dishi na County unaoendeshwa na utawala wa Gavana huyo.

Wakati huohuo, kamati hiyo imewataka Magavana 29 kufika mbele yake kujibu masuali kuhusiana na matumizi ya fedha katika kaunti zao husika, wakionya kuwa watakaokosa kufanya hivyo watakiona cha mtema kuni.

Kumekuwa na mivutano kati ya Maseneta na Magavana kwa muda sasa, huku Magavana wakiwatuhumu Maseneta kwa kutumia kamati za bunge kuwatapeli.

Ni madai ambayo Maseneta wamekanusha vikali wakiyataja kuwa yasiyokuwa na msingi.

Kulingana nao, Magavana wanatafuta kisingizio cha kutowajibishwa kuhusiana na matumizi ya fedha baada ya Mkaguzi Mkuu kutilia shaka matumizi hayo.

Share This Article