Jaji Mkuu Martha Koome amekitaja kifo cha Jaji wa Mahakama Kuu Daniel Ogembo kuwa pigo kwa idara ya mahakama.
Kifo cha Jaji Ogembo kinaifanya kuwa tatu idadi ya maafisa wa idara ya mahakama ambao wamefariki katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu David Majanja aliyefariki wakati akifanyiwa upasuaji katika hospitali moja jijini Nairobi na Hakimu Mkuu Monica Kivuti aliyepigwa risasi na kuuawa katika mahakama ya Makadara.
“Tulipokea taarifa hizo wakati tukitoa heshima zetu za mwisho kwa Jaji Majanja katika kanisa la Friends International Centre, kwenye barabara ya Ngong,” alisema Jaji Koome wakati akitangaza rasmi kifo cha Jaji Ogembo.
“Kifo cha ghafla cha Jaji Ogembo kinakuja wakati ambapo idara ya mahakama, Tume ya Huduma za Majaji na taifa kwa jumla zinakabiliwa na wakati mgumu. Hili ni pigo kubwa kwa idara ya mahakama, familia ya wanasheria na nchi yetu. Sote tumefadhaishwa,” aliongeza Jaji Koome wakati akituma risala za rambirambi kwa familia ya mwendazake.
Jaji Ogembo alijiunga na idara ya mahakama kama hakimu mnamo mwaka wa 2004 na kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mnamo mwaka wa 2016.
Hadi kufikia wakati wa kifo chake, Jaji Koome alisimamia Mahakama Kuu ya Siaya.
Jaji Ogembo alipatikana akiwa amefariki nyumbani kwake katika kaunti ya Siaya.