Martha Koome atuzwa kiongozi bora wa kike Afrika

Tom Mathinji
1 Min Read
Jaji Mkuu Martha Koome atuzwa kiongozi bora wa kike Afrika mwaka 2023.

Jaji mkuu Martha Koome Ijumaa usiku alitunukiwa tuzo ya kiongozi bora wa kike barani Afrika wa mwaka 2023, katika hafla iliyoandaliwa jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Koome alituzwa kutokana na uongozi wake wa kupigiwa mfano za kuifanyia mabadiliko idara ya mahakama hususan kutekeleza usawa wa kijinsia na kuimarisha mfumo mzima  wa sheria.

Huku akipokea tuzo hiyo, Jaji huyo Mkuu alisema tuzo hiyo haijatokana na bidii zake peke yake, mbali ni ushirikiano na wahusika wengine kwa manufaa ya maendeleo ya bara Afrika.

“Tuzo hii sio yangu peke yangu. Ni sifa ninayojitolea kwa moyo wote kwa taasisi niliyobahatika kuongoza, Idara ya Mahakama ya Kenya,” Koome alisema.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Koome alielezea umuhimu wa kuwekwa juhudi za maendeleo ya Afrika, na kubuniwa kwa mifumo na taasisi zinazojali masilahi ya wote.

“Kutambuliwa huku kunatuchochea kuendelea kutafuta uongozi bora na kuongeza bila kuchoka ubora wa utoaji wa huduma kwa taasisi zetu,” Koome alisema.

Tuzo hiyo ya kiongozi bora wa kike barani Afrika, huwatambua watu wanaochangia katika ufanisi Barani Afrika kwa kuwapa motisha viongozi wa siku zijazo na kuleta mageuzi ya Afrika katika jukwaa la kimataifa.

Website |  + posts
Share This Article