Martha Koome akashifu utekaji nyara wa waandamanaji

Tom Mathinji
1 Min Read
Jaji Mkuu Martha Koome.

Jaji Mkuu Martha Koome ameelezea wasiwasi wake kuhusu madai ya kutekwa nyara kwa baadhi ya  waandamaji, wanaoshiriki maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Koome alisema hatua hiyo inayotekelezwa na watu ambao hawajitambulishi, na wasio wawasilisha waliotekwa nyara mahakamani, ni ukiukaji mkubwa wa sheria, haki za binadamu na kinyume cha katiba.

“Katiba yetu inawataka wanaolinda sheria, kufanya kazi kwa kuzingatia haki za binadamu jinsi ilivyo kwa sheria,” alisema Jaji Mkuu.

“Sehemu ya 49 ya katiba inafafanua haki ya watu waliotiwa nguvuni, ikiwa ni pamoja na haki ya kufahamishwa sasabu ya kukamatwa, kuwasiliana na wakili na kufikishwa mahakamani katika muda wa saa 24 baada ya kukamatwa,” aliongeza Koome.

Alizitaka asasi zote za utoaji haki kuzingatia sheria zinapotekeleza majukumu yao, kwa kuhakikisha hatua zao zinawiana na katiba na sheria.

“Nahimiza asasi zote za utoaji haki kuwashughulikia wahalifu wote kwa mujibu wa sheria na kuchunguza na kushughulikia madai ya utekaji nyara wa waandamanaji haraka iwezekanavyo,” alisema Jaji Mkuu.

Aidha aliwataka wakenya wote kuzingatia katiba na mfumo wa sheria uliopo hapa nchini.

Matamshi ya Koome yamejiri baada ya madai kuibuliwa kuhusu kutekwa nyara kwa waandamanaji, wanaoshiriki maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha 2024.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *