Aliyekuwa Mama wa Taifa Margaret Kenyatta leo Jumatatu amefungua rasmi Mkutano wa Kimataifa wa kila Mwaka wa Round Square, (RSIC) unaofanyika katika ukumbi wa Bomas.
Mkutano huo wa 55 unaendeshwa na wanafunzi wenye umri wa miaka 16-18.
Ni mkutano unaofanywa kote duniani huku wanafunzi kutoka shule mbalimbali wakiwa wenyeji kila wakati.
Mkutano wa RSIC2023 unaandaliwa na shule ya Brookhouse na umewaleta pamoja wanafunzi 1,200 na walimu wao kutoka mataifa 50 katika mabara 6.
Mkutano huo ambao kaulimbiu yake ni “Afrika Mpya” unatoa fursa kwa washiriki kutafuta njia ambazo bara la Afrika limebadilika na kuelezea msimamo wake katika karne ya 21.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mama Margaret aliwakaribisha washiriki wote nchini wakati wakijiandaa kujifunza mengi kuhusu Kenya na Afrika.
“Karibuni Kenya, natumai mtajihisi nyumbani katika nchi yetu nzuri. Tunatizamia kusikia mitazamo adimu ambayo mtaleta kwa maajadiliano haya muhimu”, alisema Mama Margaret.
Alisisitiza umuhimu wa kujifunza kupitia kushiriki katika huduma kwa jamii, mipango ya mabadilishano na miradi kama ile iliyopangwa kufanyika wakati wa tukio hilo la wiki nzima.
“Tunaonaa kizazi jasiri na chenye maono kikichipuza. Nyinyi ni kizazi chenye shauku ya kutumia fursa zilizopo, kufuata ndoto zenu. Mko tayari kuhoji, kufanyia majaribio mawazo mapya, kuwa wabunifu na hatimaye kujenga dunia bora”.
Aliyekuwapo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa RSIC2023 ni Mwenyekiti na Afisa Mtendaji wa Round Square Kurt Hahn na bingwa wa Marathoni Duniani ambaye pia ni Balozi wa Amani wa Umoja wa Mataifa Tegla Loroupe miongoni mwa wengine.