Aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Kenya marehemu Jenerali Francis Ogolla, alikumbukwa jana kwenye hafla ya kusherehekea miaka 60 ya uwepo wa jeshi la wanahewa.
Katika hafla hiyo iliyoandaliwa katika kituo cha jeshi la wanahewa cha Eastleigh jijini Nairobi, Ogolla alikumbukwa kwa upanga mdogo kwa ajili ya mafanikio yake na kujitolea wakati akihudumu katika jeshi la wanahewa nchini.
Mwanawe Ogolla kwa jina Joel Rabuku ndiye alipokea upanga huo mdogo kwenye sherehe iliyoongozwa na Rais William Ruto na waziri wa ulinzi Aden Duale.
Jenerali Ogolla alifariki kwenye ajali ya ndege aina ya helikopta na wenzake 9 huko Sindar, katika kaunti ya Elgeyo Marakwet Aprili 10, 2024.
Alikuwa amehudumu kama mkuu wa majeshi ya Kenya kuanzia Aprili 2023 na alijiunga na jeshi la wanahewa mwaka 1984. Alianza kama afia wa kiwango cha pili katika jeshi hilo na baadaye akapokea mafunzo ya urubani wa vita kutoka kwa jeshi la Marekani.
Mwaka 2018, aliteuliwa kuwa kamanda wa jeshi hilo la wanahewa na baadaye naibu jenerali mkuu wa majeshi ya kenya.
Rais William Ruto alimteua kama jenerali mkuu baada ya aliyekuwa jenerali mkuu Robert Kibochi kustaafu Aprili 2023.