Mwanamuziki wa Uganda Bebe Cool na mchekeshaji Alex Muhangi wamekuwa marafiki wa muda mrefu lakini sasa urafiki umezorota kiasi cha kufikishana mahakamani.
Tatizo lilianza pale ambapo Muhangi ambaye anaendesha onyesho la vichekesho la kila wiki kwa jina Comedy Store alimwalika Bebe Cool kuja kutumbuiza kwenye mojawapo ya matamasha yake ya vichekesho mwezi februari mwaka huu wa 2025.
Cool alifika katika eneo la tukio mapema akiwa ameandamana na mkewe lakini akaondoka bila kutumbuiza jambo lililoshangaza wengi ambao walikuwa wamefika kufurahia muziki wake na vichekesho.
Anadaiwa kufanya hivyo kutokana na madai kwamba hakuwa amelipwa pesa zote kwa ajili ya tumbuizo hilo walivyokubaliana na Muhangi.
Baadaye Muhangi alielezea kwamba alikuwa ameondoka kidogo kwenye eneo hilo kwenda kumletea Bebe Cool pesa zilizokuwa zimesalia na aliporejea akapata ameshaondoka.
Mwanamuziki huyo anadaiwa kuendelea kumdai Muhangi pesa zilizosalia hata ingawa hakutekeleza sehemu yake ya mkataba wao.
Alipoona hapati pesa hizo, Bebe Cool aliwasilisha kesi mahakamani akidai kwamba Muhangi alikuwa amekiuka hakimiliki yake kwa kuchapisha video zake akitumbuiza jukwaani kwenye majukwaa ya mitandaoni ya Comedy Store.
Jana Muhangi alithibitisha kwamba amepelekwa mahakamani kupitia mtandao wa X huku akiwataka wafuasi wake wamfuate kama njia ya kusimama naye.
“Kama wengine wenu mnavyofahamu, ninakumbwa na suala la kisheria na Bebe Cool kuhusu video za Comedy Store za matumbuizo yake ambazo nilichapisha mitandaoni.” aliandika Muhangi.
Aliendelea kusema kwamba Cool alitekeleza vitisho vyake na kwamba anafaa kufika mahakamani Jumatano Machi 19, 2025 asubuhi.
“Tafadhali jiunge nami iwapo unaweza.” aliandika mchekeshaji huyo huku akiomba wale ambao wanaweza kumsimamia kama wadhamini wabebe hati stahiki kama kitambulisho.
Kesi hiyo ilianza leo asubuhi katika mahakama ya City Hall jijini Kampala na alipofika huko, Muhangi alisema hatatishwa na madai dhidi yake na kwamba atapambana hadi mwisho.