Wanafunzi zaidi ya 60 wa shule ya upili ya wasichana ya Eregi ambayo iko katika kaunti ya Kakamega wamelazwa katika hospitali mbalimbali baada ya kuugua maradhi ambayo hayajabainishwa.
Wasichana wapatao 30 wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya Kakamega, 20 katika hospitali ya Shibwe na wengine 12 wamelazwa katika hospitali ya Iguhu.
Waliohojiwa walisema walihisi wanakufa ganzi miguu na kushindwa kutembea, kupooza ambako kunakisiwa kutokana na hali ya ukosefu wa usawa kati ya chembechembe za madini zipatikanazo kwenye maji ya mwili na damu, labda kutokana na kuendesha na kutokwa jasho kwa wingi.
Kuna hofu ya idadi ya waathiriwa wa hali hiyo kuongezeka.
Hiki ni kisa cha pili cha maradhi yasiyoeleweka kukumba shule ya wasichana katika eneo hilo baada ya wanafunzi wawili na mwalimu mmoja kuaga dunia na wanafunzi zaidi ya 500 kuathirika.