Mapiganao makali yalizuka kati ya makundi pinzani ya kijeshi katika baadhi ya sehemu za mji mkuu wa Sudan, Khartoum jana Jumatano, kwani makubaliano ya kusitisha vita kwa saa 72 yaliyokiukwa mara kadhaa yamemalizika, mashuhuda wanasema.
Muda mfupi kabla ya makubaliano hayo kumalizika saa 12 asubuhi, mapigano yaliripotiwa katika miji yote mitatu ambayo inaunda sehemu kubwa ya mji mkuu wa Khartoum.
Jeshi la Sudan na kundi lenye hadhi ya kijeshi la Rapid Support Forces (RSF) yamekuwa yakipigana kwa zaidi ya miezi miwili na kusababisha uharibifu mjini Khartoum, kusababisha machafuko makubwa katika eneo la Darfur na kusababisha watu zaidi ya milioni 2.5 kukimbia makwao.
Mashambulio ya wanamgambo wanaohusishwa na RSF katika mji wa magharibi wa El Geneina yameelezewa na waangalizi wa ndani ya nchi hiyo na wa kimataifa kuwa ya kikabila.
Mashuhuda wamesema ndege ya kijeshi ilitekeleza mashambulizi ya angani katika eneo la Bahri na RSF iliitikia kwa ndege ya kukabiliana na mashambulizi hayo. Moshi ulionekana ukifuka kutoka eneo hilo la kiviwanda.
Mashuhuda pia waliripoti ufyatulianaji wa risasi na makabiliano makali katika eneo la Omdurman na mapigano ya chini ya ardhi kusini mwa Khartoum.
Wakazi pia waliripoti makabiliano karibu na makao makuu ya jeshi katika mji wa Dalanj huko Kordofan Kusini, ambako SPLM-N ikiongozwa na Abdelaziz al-Hilu, hili likiwa kundi kubwa la waasi lisiloegemea bayana upande wowote wa pande zinazozozana, limekuwa likijikusanya.
Katika taarifa, jeshi la Sudan lilimlaumu al-Hilu kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha vita na kusema kundi hilo lilikumbwa na hasara kadhaa.
Kundi la RSF pia lilishambulia kambi nyingine ya kijeshi katika sehemu nyingine ya mji huo jana Jumatano, kwa mujibu wa mashuhuda.
Makubaliano hayo yalikuwa ya hivi karibuni katika makubaliano kadhaa ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani katika mji wa Jeddah.
Kama ilivyoshuhudiwa katika makubaliano ya awali, kulikuwa na ripoti za makubaliano hayo kukiukwa na pande zote.
Chanzo: CGTN