Mapenzi yasababisha kifo Kakamega

Marion Bosire
3 Min Read

Wingu la simanzi limetanda katika kijiji cha Shinyulu eneo bunge la Khwisero, kaunti ya Kakamega baada ya askari kuwafwatulia risasi vijana wawili na kuua mmoja papo hapo walipokuwa wameenda kuwachukua wapenzi wao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo hilo, inadaiwa kuwa Boaz Katiech na Daniel Kochwa wenye umri wa miaka 28 na 21 mtawalia wakitumia pikipiki, waliondoka kijijini mwao saa tano usiku wa tarehe 27 mwezi huu kuwachukuwa vipusa wao waliohudumu kwenye baa iliyoko kijiji jirani cha Khwisero baada ya kuahidiana kufanya hivyo.

Kabla ya kuwasili, walevi waliojihami kwa silaha butu walivamia baa wanamohudumu wanadada hao hivyo kusababisha polisi kuitwa na kuwafurusha kisha wakaendelea kushika doria nje ya baa hiyo.

Muda mfupi baadaye, warembo hao walifunga kazi na kuelekea kwenye makazi yao yaliyoko mita chache na ambako Katiech na Kochwa walikuwa wanawasubiri huku wakiwa wamekaa kwa pikipiki nje ya makazi hayo.

Kwa umbali, askari mmoja aliwaona na kuwafyatulia risasi na kumuua Kochwa papo hapo huku Katiech ambaye amelazwa katika hospitali ya Butere akibahatika kuhepa ila kwa majeraha makali ya risasi sita.

Tukio hilo lilimghadhibisha mpenzi wa Kochwa–Montana Adhiambo aliyeshangaa jinsi polisi walivyofwatua risasi bila kufahamu kwa kina wanayemlenga. Vile vile, mpenziwe katiech-Jane Angelina alishangaa jinsi askari hao walivyotumia risasi kwa wapenzi wao ila hawakutumia dhidi ya walevi watundu.

Babake marehemu, Albert Atulo, aliomboleza mwanawe kwa kumtaja kuwa mtiifu na nguzo kuu kwa familia.

Kisa hicho kimeibua hisia kali kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu na maafisa wa tume huru inayoangazia utenda kazi wa maafisa wa polisi-IPOA, waliotaka hatua madhubuti kuchukuliwa.

“Hatutapumzika. Lazima tuhakikishe haki imetendeka kwa kijana aliyeuawa na anayeuguza majeraha’’, alisema mkuregenzi wa Samrin Integrated Educational Support progamme, Brenda Kusa.

Hata hivyo, taarifa ya kitengo cha polisi wa upelelezi wa Khwisero ziliarifu kuwa askari hao walikuwa wanakabiliana na jaribio la wizi wakati wa kifo hicho baada ya kupokea simu ya msaada kutoka kwa Montana Adhiambo aliyedai kuvamiwa nyumbani kwake na wanaume watano.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Khwisero James Momanyi, alisema kuwa polisi wameanzisha uchunguzi wa kina wa mkasa huo.

Share This Article