Maoni yazidi kutolewa kuhusu kisa cha Seneta Orwoba

Marion Bosire
2 Min Read

Baada ya bunge la Seneti kuamua kumpa Seneta Gloria Orwoba adhabu ya kutohudhuria vikao kwa muda wa miezi sita, maoni yamekuwa yakimiminika kuhusu suala hilo.

Aliyekuwa Seneta wa kaunti ya Mandera Billow Kerrow anahisi kwamba huenda Seneta Orwoba akapoteza wadhifa wake kama Seneta.

Akizungumza katika mahojiano, Kerrow alisema kwamba adhabu aliyopatiwa Orwoba ndiyo kubwa zaidi ambayo amewahi kuona ikitolewa dhidi ya mbunge.

Kerrow anasema iwapo Seneta huyo atakosa kuhudhuria vikao vinane mfululizo, usimamizi wa Seneti huenda ukatangaza wadhifa wake kuwa wazi.

Kwa upande wake, aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama cha UDA Kipruto Arap Kirwa amemtetea Orwoba akisema kwamba hatua iliyochukuliwa dhidi yake huenda ikamharibia kazi.

Kirwa anahisi Seneti ingepungza adhabu hiyo lakini anatumai kwamba bunge la Seneti litakuwa na likizo ndefu ili kuhakikisha kwamba Orwoba hapotezi wadhifa wake.

Na katika muda huo, anatumai Orwoba atajirudia na kujifunza kutokana na makosa yake.

Seneta Gloria Orwoba aliteuliwa na chama cha UDA na amejipata pabaya baada ya kudai kwamba wasimamizi fulani wa bunge la Seneti wa kiume walitaka uhusiano wa kimapenzi naye na alipokataa akawa anabaguliwa.

Kwenye video aliyochapisha mitandaoni, Orwoba anasema hakupatiwa muda wa kujitetea na kwamba kikao cha kujadili kesi yake kiliandaliwa bila uwepo wake kimakusudi.

Katika video hiyo, anamtaja karani wa bunge la Seneti Jeremiah Nyengenye akisema ndiye alikuwa akimnyemelea.

Bunge la Seneti liliafikia uamuzi wa kunwondoa Orwoba kwa miezi sita kwa kile kilichotajwa kuwa kutoweza kuthibitisha madai dhidi ya Nyengenye.

Hata hivyo, amesema kesi hiyo inaendelea mahakamani.

Website |  + posts
Share This Article